Jumapili 22 Machi 2026 - 15:55
Kwa nini nchi inayojitetea ya Iran, mnaiita mvamizi?/ Je, kupuuza uhalifu wa Marekani na Israel ni uadilifu?

Hawza/ Ayatollah Alireza A’rafi, mkurugenzi wa vyuo vya elimu ya dini nchini Iran (Hawza), katika barua aliyomwandikia Sheikh wa Al-Azhar, Dkt. Ahmad al-Tayyib, pamoja na kuomba kupitiwa upya tamko la hivi karibuni lililotolewa na taasisi hiyo, alisisitiza kwamba; Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inajilinda yenyewe na akataja kupuuzwa kwa uhalifu wa Marekani na Israel dhidi ya watu wa Iran kuwa ni “kuporwa kwa uadilifu na mizani ya kisheria ya dini.”

Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, kufuatia tamko la hivi karibuni la uongozi wa Al-Azhar kuhusu maendeleo yanayoendelea katika eneo hili, mkuu wa vyuo vya elimu ya dini nchini Iran alitoa tamko kwa lugha ya Kiarabu akimlenga Sheikh wa Al-Azhar. Katika tamko hilo alisisitiza umuhimu wa kuusoma mzozo wa sasa katika muktadha wake wa kihistoria na kiustaarabu, na akabainisha kwamba; Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haikuwa mwanzilishi wa mzozo huo, bali baada ya mashambulizi ya mara kwa mara, inajitetea kulinda mamlaka na heshima ya taifa lake.

Tarjama ya matini ya tamko ni kama ifuatavyo:

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu

{Wameruhusiwa kupigana wale wanao pigwa vita kwa sababu wamedhulumiwa - na kwa yakini Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwasaidia}
[Hajj: 39]

Imam Mkuu, Sheikh wa Al-Azhar, Mwenyezi Mungu amhifadhi na amlinde, Amani iwe juu yenu, rehema za Mwenyezi Mungu na baraka zake.

Na baada ya hayo:

Kwa kuwa jukumu la kisheria na kimaadili linatulazimisha sote kuwafanyia wema kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake na viongozi wa Waislamu na umma wote, na pia kutokana na upendo na kuthamini taasisi yenye mizizi mirefu ya Al-Azhar ambayo kwa karne nyingi imekuwa alama ya elimu ya wastani na mtazamo uliong’aa na imeuunganisha umma katika neno moja, tunawasilisha kwenu maneno haya machache.

Tunathamini na kusifu misimamo yenu yenye hekima na ufahamu katika masuala nyeti ya hatima ya umma, na tunajua vyema juhudi zenu zenye baraka katika kuisaidia dhamira ya Palestina, kutetea haki za watu waliodhulumiwa wa Palestina, kuhimiza umoja katika safu za Kiislamu na kukurubisha madhehebu, na kuimarisha maadili ya udugu wa Kiislamu ambao bila huo umma hauwezi kusimama. Msimamo huu adhimu tuliouzoea kutoka kwenu umetufanya tusimame kwa muda mrefu mbele ya tamko la hivi karibuni la Al-Azhar kuhusu maendeleo ya sasa katika eneo, na tunawaombeni kwa dhati kulipitia upya kwa kuzingatia ukweli mkubwa ambao hauwezi kupuuzwa katika hukumu yoyote ya kisheria, kisiasa au kimaadili.

Kwanza: Ufahamu sahihi wa mapambano yanayoendelea leo hauwezekani bila kuzingatia muktadha wake wa kihistoria na kiustaarabu. Kinachoshuhudiwa katika eneo ni sehemu ya mnyororo wa mgongano wa kiustaarabu na mradi wa kikoloni wa Magharibi—wa Marekani—ambao tangu zamani unalenga kuunda upya ramani ya eneo kwa maslahi yake, kudhoofisha uwezo wa umma, na kuamsha migogoro midogo inayotupotosha kutoka kiini cha mzozo, ambacho ni mradi wa kutawala mali na maeneo matakatifu ya umma wa Kiislamu na kulinda utawala wa Kizayuni kama ncha ya mkuki wa mradi huu katika moyo wa ulimwengu wa Kiislamu.

Pili: Kwa mtazamo wetu, suala la Palestina bado ndilo suala kuu la umma huu. Mateso ya miaka themanini ya watu wa Palestina kutokana na uvamizi, dhulma, kufukuzwa, ujenzi wa makazi na kufanya maeneo matakatifu kuwa ya Kiyahudi ni jeraha linalovuja damu linaloumiza dhamiri ya umma, na tafsiri yoyote ya matukio inayopuuza ukweli huu imepuuza sababu kuu na kushughulikia matokeo yake.

Tatu: Tunakufahamisha wewe na umma wote wa Kiislamu kwa msisitizo kwamba; imani thabiti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika umoja na udugu wa umma na mshikamano wa kina kwenye ukanda si kauli tu, bali ni msingi wa sera na mipango ya vitendo ambayo tumefuata kwa miongo kadhaa na tunaendelea kuwa waaminifu kwayo.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu ailinde Al-Azhar kama alama ya elimu na uadilifu, awaongoze wote kwenye njia sahihi, na auunganishe umma katika haki, kwani Yeye ndiye Msimamizi wa hilo na Muweza juu yake.

Na amani iwe juu yenu na rehema za Mwenyezi Mungu na baraka zake

Alireza A’rafi

Mkuu wa vyuo vya elimu ya dini nchini Iran

Inafaa kutajwa kwamba, uongozi wa Al-Azhar katika tamko lake lililotolewa Jumanne tarehe 26 Esfand 1404 (17 march 2026), ulilaani radi amali ya kijeshi ya Iran dhidi ya mashambulizi ya Marekani na Israel, na kuitaka Iran kusitisha mara moja kile ilichokiita “mashambulizi yasiyo na sababu dhidi ya nchi za Kiarabu na Kiislamu,” na ukaonya kuhusu athari zake hatari kwa usalama wa eneo na maisha ya raia.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha